Social Icons

Pages

Friday, November 22, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



          Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), linapenda kukanusha taarifa zilizoandikwa kwenye Gazeti la ‘The Citizen’ la tarehe 20 Novemba 2013 toleo Nambari 2980 lililochapishwa kwenye ukurasa wa 15 kwa kichwa cha habari ‘From genocide suspects to a DRC rebel faction – 2’

Katika taarifa hiyo, mwandishi ametoa tuhuma za uongo dhidi ya Maafisa wa JWTZ alizozinukuu kutoka ripoti ya wataalam wa Umoja wa Mataifa( UN Group of Experts Report). Kwa mujibu wa tuhuma hizo, imeelezwa eti kuwa  baadhi ya makanda wa JWTZ wanakisaidia kikundi cha FDLR. Tuhuma hizo ziliwahi kukanushwa kuwa hazikuwa za ukweli.

JWTZ linarudia kukanusha tuhuma hiyo na kusisitiza kwamba hakuna Afisa wake  yeyote aliyepo kwenye Utumishi ambaye amejihusisha au kuwa na ushirikiano na kikundi cha FDLR.  Pia, hakuna ushahidi wowote wa kuonesha kuwa Maafisa wa JWTZ waliostaafu ama wamewahi kushirikiana au wanaendelea kushirikiana na kikundi  hiki.

Aidha,  hakuna Makamanda wa JWTZ waliopo kwenye Jeshi la Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO-FIB) ambao wamejihusisha kufanya mazungumzo au kushirikiana na kupanga mpango wowote na kikundi cha FDLR.

Tuhuma hizo zilizotolewa na mwandishi huyo ni za uongo na zinalenga kuchafua sifa na rekodi nzuri ya JWTZ na Tanzania kwa ujumla.
Kama inavyofahamika Tanzania imepeleka kikosi chake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama sehemu ya FIB chini ya MONUSCO. Jukumu la FIB ni kusaidia kurejesha Amani eneo la Mashariki, nchini DRC na hivyo kukabiliana na vikundi mbalimbali vyenye silaha vinavyotishia amani na usalama katika eneo hilo.  FDLR ni sehemu ya vikundi hivyo.
Hivyo inashangaza sana kuona kuwa pamoja na jukumu hilo muhimu linalofanywa na kikosi cha Tanzania bado tuhuma hizo zinatolewa na mwandishi huyo.

JWTZ litaendelea kutekeleza wajibu wake ipasavyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa nidhamu ya hali ya juu, weledi na uadilifu kama ilivyo kawaida yake na kwa mujibu wa Azimio lililotolewa na Umoja wa Mataifa na pia kwa mujibu wa maamuzi, malengo na matarajio ya Kanda ya Maziwa Makuu, SADC na AU.


Imetolewa  na  Kurugenzi  ya  Habari  na  Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga

S.L.P  9203,   Dar es Salaam, Tanzania.

No comments:

Post a Comment

 

Sample text

Sample Text

Sample Text