Benki Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender) zinazotumika nchini. Katika kutekeleza jukumu hili Benki Kuu hutengeneza noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denominations) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawika katika zile zenye thamani ndogo ndogo.
Hii hulenga kurahisisha upatikanaji wa chenji na uwezekano wa wahitaji wa viwango mbalimbali vya bidhaa na huduma kupata katika mafungu yatakayokidhi mahitaji yao.
Katika kutekeleza jukumu hili, Benki Kuu imetoa toleo jipya la Sarafu ya Shilingi 500. Hatua hii imezingatia yafuatayo:
• kwamba noti ya shilingi mia tano (500), ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida ya kila siku ya wananchi wengi kuliko noti nyingine yoyote. Hivyo noti hiyo hupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi sana na kuchakaa haraka.
• Noti hizi hukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe zinapokuwa zimefikia ukomo wake.
• Sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi kuliko noti.
Sarafu hii inatambuliwa kwa kuangalia yafuatayo:
• Umbo lake ni la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5
• Ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma (Steel) na “Nickel”
• Kwa mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani.
• Ina alama maalum ya usalama iitwayo “latent image” iliyopo upande wa nyuma ambayo ni kivuli kilichojificha. Kivuli hiki huonesha thamani ya sarafu ‘500’ au neno ‘BOT’ inapogeuzwa-geuzwa.
Sarafu hii mpya ya shilingi mia tano (500) inatarajiwa kuingizwa kwenye mzunguko kuanzia mwezi Oktoba 2014.
Sarafu hii, itakuwa ikitumika sambamba na noti zilizopo sasa za shilingi mia tano mpaka hapo noti hizo zitakapokwisha katika mzunguko.
Pamoja na taarifa hii; tunawaomba wananchi kuendelea kufuatilia vipindi mbalimbali vitakavyokuwa vinaeleza jinsi sarafu hii ilivyo na namna ya kutunza noti na sarafu zetu kwa njia salama.
Ahsanteni Sana