Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kukanusha taarifa za uvumi zinazosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo vya habari kuwa kuna Watanzania wapatao 160 wamenyongwa nchini China kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya.
Wizara inapenda kuujulisha Umma kuwa hakuna Mtanzania yeyote aliyenyongwa kama inavyodaiwa kwenye mitandao na vyombo vya habari.
Aidha, taarifa hiyo ya uvumi imedai kuwa ndugu wa mmoja wa Watanzania hao ambaye kwa jina anajulikana kama Bw. Rajab Mohamed Ismail Mapusa wamekaa matanga kuomboleza kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Serikali ya China, Bw. Mapusa yupo hai gerezani akitumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kuingiza madawa ya kulevya nchini humo, na hivi karibuni alishiriki kuandaa maonyesho ya utamaduni wa Kiafrika wakati wa kuadhimisha sherehe za Mwaka Mpya wa China.
Wizara inapenda kuwakumbusha Wanahabari kuandika taarifa ambazo ni sahihi zisizopotosha Umma kwa kuzingatia weledi, maadili na ukweli kutoka mamlaka zote husika.
Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
10 Februari, 2014